Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Metamaywa ilioko katika eneo Bunge la Kitutu Masaba Kaunti ya Nyamira amewaomba wahisani kuwasaidia katika ujenzi wa vyoo.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Hii ni baada ya vyoo vilivyokuwa katika shule hiyo kuharibiwa na mvua inayoendelea kunyesha katika eneo hilo.

Maafisa wa afya waliamrisha kufungwa kwa shule hiyo hadi pale ambapo itajenga vyoo hivyo.

Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumanne kwa njia ya simu, mwalimu mkuu huyo Monicah Moraa alisema wanahitaji shilingi elfu mia sita ili kujengea vyoo hivyo.

 Alisema kiasi cha shilingi elfu mia mbili walichopatiwa na hazina ya ustawi ya maeneo bunge maarufu CDF katika eneo bunge hilo ni cha chini mno na hivyo kuwaomba wahisani kuingilia kati ili wanafunzi waweze kurejelea masomo ya muhula wa pili.

“Maafisa wa afya walisema ni lazima tujenge vyoo kabla ya kufungua shule. Kwa hivyo tunawaomba wahisani kutusaidia katika ujenzi wa vyoo hivyo ili wanafunzi waweze kurejelea masomo. Tulipatiwa Sh200,000 na hazina ya CDF kupitia kwa mbunge Timothy Bosire huku bajeti ya ujenzi wa vyoo ikiwa Sh 600,000,” alisema mwalimu mkuu huyo.

Alisema imekuwa vigumu kuendelea na masomo bila pahali pa kujisaidia iwapo wanafunzi hao watahisi kuenda haja.

Moraa alisema kuwa wanafunzi hao wakiendelea kukaa nyumbani itaathiri matokeo ya mtihani wa kitaifa na hivyo kuitaka serikali kuingilia kati.

Vyoo hivyo viliharibiwa na mvua mwanzoni mwa muhula huu. Shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 240 kulingana na mwalimu mkuu huyo.