Jengo la Mahakama ya Mombasa.[Picha/ the-star.co.ke]
Mahakama ya Mombasa imemuachilia huru Sheikh Khalid Mohammed, mwalimu wa dini ya Kiislamu, aliyekuwa akikabiliwa na madai ya ugaidi.Khalid, ambaye alikuwa imamu katika msikiti wa Mlango wa Papa jijini Mombasa, anadaiwa kutenda makosa hayo mnamo Mai 20, 2015 katika makaazi yake eneo la Bondeni na Tudor.Khalid amekaa kizuizini kwa muda wa miaka miwili sasa.Alikuwa anakabiliwa na mashtaka ya kuwa na uhusiano na kundi la al-Shabaab, kumiliki vilipuzi na kanda za video zenya mafunzo ya ugaidi na kutoa mafunzo ya itikadi kali.Aidha, alikabiliwa na shtaka la wizi wa gari ambalo linadaiwa kuhusika katika shughuli za kigaidi.Akitoa uamuzi huo siku ya Alhamisi, Hakimu Henry Nyakweba alimuachilia huru Sheikh Khalid baada ya kukosekana kwa ushahidi wa kutosha wa kumuhusisha na madai hayo.“Hakuna ushahidi mwafaka uliotolewa ambao unamuhusisha mshukiwa huyo na madai hayo, kwa hivyo sioni sababu ya kumfunga gerezani,” alisema Nyakweba.Nyakweba alisema kuwa polisi pamoja na afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma imeshindwa kuwasilisha ushahidi wa kutosha dhidi ya madai hayo.“Polisi pamoja na afisi ya mwendesha mashtaka wameshindwa kuwasilisha ushahidi wa kutosha mbele ya mahakama hii. Ushahidi uliowasilishwa mahakamani ni hafifu mno,” alisema Nyakweba.Hakimu huyo alitilia shaka vilipuzi vinavyodaiwa kupatikana kwenye nyumba ya mshukiwa huyo na kusema kuwa huenda vilipilekwa humo na polisi waliofanya upekuzi katika nyumba ya Khalid.“Inaonekana hivi vilipuzi vinavyodaiwa kupatikana katika nyumba ya mshukiwa viliwekwa humo kwa sababu mshukiwa hakuhusishwa katika upekuzi uliofanywa katika nyumba yake,” alisema Nyakweba.Aidha, Nyakweba amewalaumu polisi kwa kuvamia nyumba ya mshukiwa huyo nyakati za usiku pasi agizo kutoka kwa mahakama, hatua aliyoitaja kama ukiukaji wa haki za mshukiwa.“Polisi walikiuka sheria kwa kuvamia na kuanza kukagua nyumba za mshukiwa pasi idhini ya mahakama. Sheria hairuhusu ukaguzi huo kufanyika usiku. Ukaguzi wa usiku unaweza kufanyika pindi tu kunapokuwa na agizo la mahakama,” alisema Nyakweba.Upande wa mashtaka ukiongozwa na Daniel Wamotsa umetishia kukata rufaa kupinga kuachiliwa huru kwa sheikh Khalid.