Mwalimu mkuu wa shule ya upili ya wasichana ya Itibo amewaomba viongozi kutoka eneo la Gusii kusaidia shule hiyo kupata vifaa vya kutosha vya kufanyia sayansi tekelezi ili kuboresha matokea ya wanafunzi wa shule hiyo katika masomo ya sayansi.
Akizungumza siku ya Jumanne katika shuleni humo katika hafla ya siku ya kuzawadi wanafunzi wa kidato cha nne waliofanya vizuri kwa mtihani wa kidato cha nne mwaka uliopita, mwalimu huyo, Rechel Mokua aliitaka hasa kamati inayosimamia maendeleo ya eneo bunge kutoka eneo hilo kuangalia suala hilo na kuwajengea maabara ya kisayansi.
“Shule yetu imekuwa ikijitahidi sana katika kufanya vizuri hasa masomo ya sayansi na tuna changamoto za vifaa vya kutuwezesha kufanya vizuri zaidi; tu tayari kutoa matokeo mema zaidia kuliko ya mwaka jana, hivyo naomba kaunti pamoja na mbunge wa hapa atufadhili,” alisihi Bi Mokua.
Hata hivyo, mwalimu aliwapongeza wanafunzi wote waliofanya vizuri mwaka jana na kuahidi kuendelea kuboresha matokeo ya elimu kwenye shule hiyo.
Shule nyingi katika eneo la Kisii zina uhaba wa vifaa na maabara, huku wakiomba serikali ya kaunti kuwasaidia kupata vifaa hivyo.