Huku shule ya msingi ya Gesere kutoka kata ya Ibeno kaunti ya Kisii ikifungwa na maafisa wa afya ya umma kutoka wizara ya afya Kisii, mwalimu mkuu wa shule hiyo Felister Onchari ameomba ufadhili kwa viongozi kutoka eneo hilo kushughulikia ujenzi wa vyoo ili wanafunzi warejee shuleni.
Shule hiyo ya Gesre, ambayo ilionywa mapema mwaka huu kujenga vyoo ambavyo vilikuwa vimechakaa, illipoteza mda wa kuvijenga na ikawabidi maafisa hao wa afya kuchukua hatua ya kuifunga hadi vijengwe.
Mwalimu huyo mkuu alijitetea kwa kusema kuwa alipotumwa kama mwalimu mkuu katika shule hiyo mwaka wa 2010, alipata shule hiyo haikuwa na vyoo, akajenga vyoo vya mda ambavyo vimekuwa vikiwahudumia wanafunzi.
Aidha, alisema kuwa udongo wa eneo hilo ni mwepesi mno na huwezi kustahimili msingi wa vyoo vya kudumu.
“Udongo wetu hapa shuleni ni mwepesi na huwa unabomoka kwa haraka, swala ambalo linakuwa gumu kwa vyoo vya kudumu, lakini natarajia kuwa tuna wahandisi watashughulikia ujenzi huo vizuri, na naomba viongozi kutupa msaada wa kujenga vyoo hivi,” alihoji Onchari.