Mwanabiashara mmoja alifikishwa mbele ya korti ya Munispaa ya Eldoret siku ya Jumatano na kushtakiwa kwa kosa la kuuza nyama haramu, mashtaka ambayo mtu huyo wa umri wa makamu aliyakubali.

Share news tips with us here at Hivisasa

Edwin Rotich alishtakiwa kwa kosa la kuuza nyama bila ruhusa kutoka kwa Wizara ya Afya ya Umma.

Korti iliambiwa kuwa mshtakiwa huyo alikuwa anauza nyama hiyo mjini Eldoret mwendo wa saa tano mchana kwa wananchi kinyume na sheria ya Wizara husika kabla ya kunaswa na maafisa kutoka kitengo cha afya wa Kaunti ya Uasin Gishu.

Alipigwa faini ya Shilingi 10,000 pesa taslimu, ambazo alizilipa kisha akaachiliwa. Kesi hiyo iliamuliwa na hakimu makazi wa korti hiyo N.N Moseti.

Kwengineko, msako mkali leo ulifanywa mjini Eldoret na kukamatwa kwa watoto wa kuranda randa mtaa ovyo na kuvuruga amani na walevi katikati mwa mji huo.

Msako huo uliongozwa na polisi wa utawala wakishirikiana na askari wa Munispaa ya mji huo.

Watu walionaswa walikua zaidi ya 40, huku wa kuranda randa mtaani wakiwa 33, wawili walikua wamelewa chakari na saba kati yao walikua chini ya umri ya miaka 18.

Vile vile, washukiwa hao wanatarajiwa kufikishwa mbele ya korti ya Munispaa ya Eldoret ili kujibu mashtaka yanayowakabili.

Kando na hayo, waliokuwa chini ya miaka 18 watapelekwa makao ya kurekebishia tabia.