Mwanablogi maarufu anayeishi katika Kaunti ya Kilifi Samir Nyundo ameenda mafichoni baada ya kupata vitisho kutoka kwa watu wasiojulikana.
Haya yanajiri baada ya Bwana Nyundo kulalamikia kuuawa kwa mwanahabari Joseph Masha.
Nyundo, ambaye ni msimamizi wa mtandao unaojulikana kama Cheche amekuwa akishinikiza idara ya usalama kufanya uchunguzi dhidi ya kifo cha mwanahabari huyo aliyekufa katika katika hali ya kutatanisha.
Akizungumza na waandishi wa habari, Nyundo alisema amekuwa akipata ujumbe wa vitisho akiambiwa kuwa atauawa.
Haya yanajiri huku idara ya upelelezi mjini Kilifi, ikiongozwa na Jason Muingi, ikisema kuwa uchunguzi kuhusu kifo cha mwanahabari huyo unaedelea.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa mashtaka ya umma Keriako Tobiko ametoa hakikisho la uchunguzi kufanywa na hatua kuchukuliwa, ili kukomesha visa vya dhuluma dhidi ya wanahabari.
Wanahabari jijini Nairobi waliandamana siku ya Alhamisi hadi katika ofisi za Tobiko kulalamikia kukithiri kwa visa vya mauji ya wanahabari kwa sababu za kikazi.