Mwanachama wa shirikisho la kitaifa la madiwani nchini Valentine Simani amejitokeza kushtumu vikali tabia ya wanaume kuwavua nguo wanawake wasiovaa vizuri hadharani. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Akiwahutubia wanahabari mjini Nyamira baada ya kuhudhuria kongamano la madiwani wa zamani kutoka eneo hilo siku ya Jumatatu,  Simani alisema kuwa haifai wanaume kuwavua nguo wanawake mbele ya umma kwa maana hali hiyo inahujumu haki zao na kuwadhalilisha mbele ya umma. 

"Hii tabia ya wanaume kuwavua wanawake nguo mbele ya umma eti kwa sababu kwamba wamevaa visivyostahili ni mbaya na kamwe haistahili kwa maana inawadhalilisha sana wanawake," alisema Simani.

Simani aidha aliitaka serikali kuwachukulia hatua za kisheria wanaume watakaopatikana na kosa la kuwavua nguo wanawake, huku akihoji kuwa sharti kina mama waheshimiwe. 

"Ni ombi langu kwa serikali kuhakikisha kuwa wanaume watakaopatikana kuhusika na kosa la kuwavua nguo wanawake wametiwa mbaroni na kukabiliwa kisheria," aliongezea Simani. 

Haya yanajiri baada ya mama mmoja kuvuliwa nguo hadharani kule Malindi kwenye uchaguzi mdogo wa cheo cha ubunge siku kadhaa zilizopita.