Familia moja huko Komboboma kaunti ndogo ya Magarini imeamkia mshangao baada ya kuupata mwili wa mvulana mwenye umri wa miaka 14 ukining'inia kwenye mti. Kulingana na walioshuhudia kisa hicho, marehemu ambaye ni mwanafunzi wa darasa la sita katika shule ya msingi ya Kaembeni, alijitia kitanzi mita chache kutoka nyumbani kwao.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mkuu wa polisi kaunti ndogo ya Magarini John Kilokwe alisema tayari polisi wameanzisha uchunguzi, lakini anahofia huenda marehemu alichukua hatua hiyo kutoakana na hali ngumu ya kimaisha.

Kilokwe alidokeza kuwa kwa muda mrefu marehemu aliishi na babake mdogo baada ya kuachwa na wazazi wake walioachana baada ya ndoa yao kuvunjika kufuatia mzozo wa nyumbani.

Na katika kisa tofauti Mzee wa miaka 65 aliuawa kwa kushambuliwa kwa panga usiku wa kuamkia Jumatatu na watu wasiojulikana katika eneo la Mdunguni kaunti ndogo ya Malindi.

Naibu chifu Joseph Lugwaru alisema ni kufuatia kisa hicho, maafisa wa usalama wakishirikiana na wazee wa nyumba kumi wameanzisha uchunguzi kuwapata wahusika. Lugwaru alisema marehemu alishambuliwa kwake nyumbani na kuaga dunia alipokuwa akipokea matibabu katika hospitali kuu ya ukanda wa Pwani.

Naibu huyo wa chifu alisema madaktari katika hospitali kuu ya kaunti ndogo ya Malindi walilazimika kumkimbiza hadi mjini Mombasa kwa matibabu maalum baada ya hali yake kuwa ngumu zaidi. Naye afisa mkuu wa upelelezi kaunti ndogo ya Malindi Jackob Ngao alisema maafisa wake wamenazisha uchunguzi.