Mwanafunzi mmoja wa Shule ya Upili alilazimika kuhairisha safari ya kurejea shuleni baada ya Manamba katika steji ya Tuskys mjini Kisii kumng'ang'ania na kumrarulia begi na nguo yake siku ya Jumanne asubuhi.
Mwanafunzi huyo ambaye alikuwa anaelekea Shule ya Wasichana ya Iterio alijipata kwenye mpapurano huo kati yake na manamba hao ambao walimvamia wakiwa zaidi ya watatu kila mmoja akimvuta kuelekea kwenye gari lake ndiposa mkoba wake uliokuwa na nguo ukakatika na nguo kudondoka chini pamoja na kuraruliwa shati lake la shule.
Kisa hicho kilizua ghadhabu kali miongoni mwa wazazi na abiria waliokuwa hapo ambao waliweza kuwashambulia wawili miongoni mwao manamba hao, lakini wakaweza kuokolewa na manamba wenzao na kutorokea maisha yao.
Hata hivyo Mwenyekiti wa magari ya Moigi Shuttle Charles Tamaro ambaye pia ni Naibu wa Katibu wa magari ya steji hiyo ya Tuskys aliahidi kuwa watawachukulia hatua ya kisheria manamba waliohusika kwenye patashika hiyo ya kuvuruga mwanafunzi huyo.
"Wengine wetu tuna watoto wa Shule kama hawa, tabia kama hii ni aibu kubwa sana. Nitachukua hatua mimi binafsi kuhakikisha wahusika wameshikwa na kupelekwa Kortini,” alionya Tamaro huku akiwataja wahusika kuwa ni vijana wana nia ya kuibia watu na wala hawajajiandikisha na Sacco yoyote ile katika Kaunti ya Kisii.
Sio mara ya kwanza abiria kulalamikia vitendo vya Manamba kutoka steji nyingi mjini humo ambapo kwa sasas wametishia kuchukua sheria mikononi mwao kama Serikali ya Kaunti ya Kisii haitachukua hatua ya kukomesha vitendo hivyo vya baadhi ya Manamba.