Share news tips with us here at Hivisasa

Mariasalus Karabu, kutoka mjini Mombasa, ameteuliwa kushiriki katika hafla ya kitamaduni inayotarajiwa kufanyika nchini Marekani.

Hafla hiyo inayoangazia makabila ya Kenya na tamaduni zao, inatarajiwa kuanza mwezi Agosti mwaka huu.

Karabu, mwenye umri wa miaka 17, kutoka mtaa wa Bamburi, ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya upili ya State House Girls mjini Nairobi.

Karabu ameteuliwa kuwakilisha kabila lake la Wagiriama katika hafla hiyo itakayodumu kwa muda wa mwaka mzima ambapo pia watapitia mafunzo mbalimbali wakiwa nchini humo.

Katika mahojiano ya kipekee na mwandishi huyu siku ya Jumatano, Karabu alisema anafurahia fursa hiyo ya kipekee na kuipokea kama zawadi kubwa kwake.

“Tuliteuliwa wanafunzi wengi kisha tukapewa mtihani na nilifurahi kuwa mmoja wa wale waliofaulu kupata ufadhili huo wa kwenda Marekani,” alisema mwanafunzi huyo.

Karabu alisema kuwa kuteuliwa kwake kumemfanya kutaka kujua asili ya jamii hiyo ya Wagiriama na kuhafamu tamaduni zake za jadi.

Aidha, alisema kuwa anatarajia safari hiyo ya nchini Marekani itamwezesha kupiga hatua kubwa katika masomo yake.

Jumla ya wanafunzi 18 kutoka humu nchini walichaguliwa kuhudhuria hafla hiyo iliyodhaminiwa na shirika la Marekani la American Field Services kwa ushirikiano na ubalozi wa Marekani.