Mwanafunzi wa chuo kikuu cha Moi amefikishwa kizimbani kwa tuhuma za kuhusishwa na mtandao wa kigaidi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Hassan kassim Hassan, alitiwa mbaroni tarehe Oktoba 31 baada ya kudaiwa kuhusika na kundi la kigaidi la ISIS.

Inadaiwa kuwa Hassan alikuwa na nia ya kusafiri hadi nchini Libya kujiunga na kundi hilo.

Afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umaa imeitaka mahakama kuagiza kuzuiliwa kwa mshukiwa huyo kwa muda wa siku 15, ili kutoa nafasi kwa maafisa wa polisi kufanya uchunguzi.

Mwendesha mashtaka Eugine Wangila aliambia mahakama kuwa mshukiwa huyo huenda akatoroka iwapo ataachiliwa kwa dhamana.

Hata hivyo, hatua hiyo ilipingwa na wakili wa mshukiwa, Mohammed Fakii, aliyehakikishia mahakama kuwa mteja wake hawezi toroka.

“Mteja wangu hawezi kutoroka. Hiyo ni njama ya kukandamiza haki za mteja wangu,” alisema Fakii.

Akiotoa uamuzi wake Hakimu Francis Kiambiia, aliagiza Hassan kuzuiliwa korokoroni kwa siku kumi.

“Katiba inaruhusu mshukiwa wa ugaidi kuzuiliwa kwa muda wa siku 90, lakini mshukiwa huyu azuiliwe kwa siku kumi pekee”, alisema Kiambia.