Mwanafunzi mmoja katika Chuo Kikuu cha Kisii alishikwa jana usiku na kuwekwa korokoroni baada ya jaribio lake la wizi kutibuka.

Share news tips with us here at Hivisasa

Hii ni baada ya jitihada zake za kuvunja mlango zilipojulikana na wanafunzi wenye bweni hilo. Walipiga usiahi uliovutia wanafunzi wengi waliojitokeza na kumkimbiza mwanafunzi huyo hadi walipomshika.

Aliokolewa na walinda usalama kwani wanafunzi walikuwa wakimnyeshea mvua ya ngumi na mateke.

Akidhibitisha tukio hilo, msimamizi wa malazi Chuoni Kisii Mong’are alisema kuwa kulikuwa na jaribio la wizi japo lilitibuka na mwanafunzi huyo amewekwa korokoni kwenye kituo cha Polisi cha Kisii Central akisubiri kufikishwa mahakamani leo (Jumanne) kwa mashitaka ya wizi ya mabavu.

“Ni kweli jana usiku mwanafunzi mmoja alijaribu kuvunja mlango katika harakati zake za kutaka kuibia wenzake japo alikabiliwa na wanafunzi wenzake. Nawashukuru wanafunzi kwa ushirikiano wao ya kuhakikisha kuwa kuna usalama hapa Chuoni. Kwa sasa mshukiwa yupo korokoroni akisubiri kufikishwa mahakamani,” alisema Mong’are.

Halikadhalika amewashauri wanafunzi kuwa wangalifu wakati huu ambao muhula unaelekea tamati kwani wizi hunawiri wakati kama huu. “Ombi langu ni kuwa wanafunzi wawe makini na mali yao,” alisisitiza Mong’are.

Wanafunzi wamelalamikia tatizo la wizi kwani hivi punde wanafunzi wameporwa vitakilishi, simu na pesa kutoka kwenye vyumba vyao.

Wameiomba idara ya malazi kuongezea usalama na kuwapa adhabu kali wanafunzi wanaopatikana kwa tuhuma za wizi.