Mwanaharakati wa maswala ya kijamii katika Kaunti ya Mombasa Hassan Mwakimako, amekosoa jinsi zoezi la kukusanya maoni ya makadario ya bajeti lilivyoendeshwa.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mwanaharakati huyo amesema kuwa wananchi hawakupewa muda wa kuchambua bajeti hiyo kabla ya kutoa maoni.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatano, mwanaharakati huyo alisema lazima wananchi wapate habari kamili kabla ya kutoa maoni yoyote.

“Kabla mwananchi apewe nafasi ya kuchangia, lazima awe na habari kamili na aelewe hiyo bajeti iko vipi,” alisema Mwakimako.

Mwanaharakati huyo alikosoa serikali ya kaunti kwa kile alichotaja kama kupanga kila kitu na kisha kuhusisha mwananchi katika hatua ya mwisho tu.

“Bajeti imepangwa alafu mwananchi anaitwa tu kwenda kuelezewa kile kimepangwa na hiyo sio sawa,” aliongeza Mwakimako.

Aidha, Mwakimako alidokeza kuwa kulingana na katiba, mwananchi anafaa kushirikishwa kuanzia mwanzo hadi zoezi hilo linapokamilika.

Zoezi hilo lilitibuka katika awamu ya kwanza pale wananchi walipotaka kujua jinsi fedha zilivyotumika katika bajeti ya awali.