Shirika la utetezi wa haki za kibinadamu nchini la Haki Africa, sasa linataka waliyotajwa kuhusika na kashfa za ufisadi katika ripoti iliyotolewa na tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini EACC kuchukuliwa hatua za kisheria.
Afisa wa maswala ya haki na sheria katika shirika hilo Francis Auma Gamba amesema kuwa ufisadi umekuwa donda sugu na Wakenya wengi hususan wale wa mashinani wakipitia changamoto huku baadhi ya watu fulani wakifaidika nchini.
Akiongea mjini Mombasa, Auma amesema kuwa kama shirika linapenda kuona wahusika wakifikishwa mahakamani na hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yao ili swala la ufisadi nchini kusitishwa na wananchi kunufaika na miradi mbalimbali ya kimaendeleo.
Wakati uo huo amemshtumu Gavana wa kaunti ya Kwale Salim Mvurya kwa kupinga ripoti ya EACC kufuatia kaunti hiyo kutajwa kuwa kaunti fisadi zaidi eneo la Pwani huku akipendezeka hatua za dharura kuchukuliwa kwa viongozi wafisadi nchini.
"Tunashangazwa na baadhi ya viongozi wakipinga ripoti ya ufisadi iliyotolewa na tume ya EACC wakisema kuwa ni ya uongo, hilo hatukubaliani nao lazima wakubali kuwa ani wafisadi na hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yao," alisema Auma.
Mwanaharakati huo wa kijamii imewashinikiza Wakenya kuhakikisha kuwa wanawaripoti viongozi na wakaazi wanafuja fedha za umma ili kuchukulia hatua na kukomesha ufisadi nchini.