Wakaazi wa eneo la Likoni, Kaunti ya Mombasa, wakiongozwa na mwanaharakati mmoja kutoka eneo hilo, wameanza mazungumzo na kampuni ya uchimbaji madini ya Base Titanium, kuishinikiza kuanza miradi katika eneo hilo.
Wakiongozwa na mwanaharakati wa haki za binadamu Mgandi Kalinga, wakaazi hao wameitaka kampuni hiyo inayochimba madini katika kaunti jirani ya Kwale, ambayo ina bohari la kuhifadhi madini eneo hilo la Likoni, kuwasaidia.
Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumanne, Kalinga alisema kuwa malori yanayobeba madini hayo kutoka Kwale kuja hadi katika eneo la Likoni, yamekuwa yakiharibu barabara hiyo kutokana na uzito.
Aidha, wameitaka kampuni hiyo kutoa fidia kwa wananchi.
Wakati huo huo, Kalinga amesema kwamba tayari amefanya mazungumzo na wasimamizi wa kampuni hiyo, na sasa watateua wakaazi kadhaa wa eneo hilo kufanya mazungumzo.
“Tumekubaliana kwamba tutachagua watu kadhaa kabla siku saba kuisha. Tutaenda hadi katika kampuni hiyo na kisha tutarudi tena na kuandaa kikao na wakaazi ili tuwaeleze kile tutakuwa tumejadili,” alisema Kalinga.
Mwanaharakati huyo ametaja miradi ya shule na maji kama baadhi ya mahitaji yanayohitajika eneo hilo.
Aliongeza kwamba kampuni hiyo imekuwa ikifanya miradi mingi Kaunti ya Kwale, lakini wakaazi wa Likoni hawajafaidika na lolote licha ya kwamba bohari kubwa zaidi la kuhifadhi madini hayo limejengwa eneo hilo.