Huku Wakenya wakielekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka ujao, wanaharakati wa kutetea haki za kibinadamu wamesema kuwa wananchi wanafaa kuhamasishwa kuhusu jinsi watakavyoshiriki kikamilifu kwenye uchaguzi huo, ili kuwawezesha kuleta mageuzi katika taifa hili.
Akizungumza siku ya Jumanne mjini Mombasa kwenye mkutano wa vijana, afisa wa haki na sheria katika shirika la kutetea haki za kibinadamu la Haki Afrika Francis Gamba, alisema kuwa wananchi wengi wamepoteza imani ya kushiriki kwenye uchaguzi mkuu ujao, kwa kuwa hawajaona mageuzi yoyote kwa viongozi waliowachagua.
Alisema kuwa kwa mara nyingi viongozi hao huishia kujinufaisha wenyewe badala ya kuleta maendeleo kwa wananchi.
"Kuna haja ya wananchi kuhamasishwa kuhusu kushiriki kwenye uchaguzi mkuu ujao ili kuleta mabadiliko katika taifa hili na kuhakikisha kuwa wanawachagua viongozi waadilifu ambao wataleta mabadiliko nchini,” alisema Gamba.
Aidha, mwanaharakati huyo alielezea umuhimu wa hamasa hiyo, kwa kusema kuwa itasaidia wananchi wengi kushiriki uchaguzi mkuu ujao na kuleta mageuzi katika uongozi wa nchi.
Wakati huo huo, aliwataka vijana hususan wa eneo la Pwani kuhakikisha kuwa wanajitenga na siasa za uchochezi zinazolenga kuwatumia vibaya na kuvuruga amani, sawia na usalama wa eneo hilo.
Aliwataka vijana kushirikiana na mashirika ya kijamii kueneza ujumbe wa amani.