Mwanaharakati wa chama cha Jubilee Janet Mirobi amesema huenda chama hicho kikakubwa na msukosuko kufuatia kutofautiana kwa viongozi kutoka Pwani.
Haya yanajiri baada ya viongozi wa chama hicho kuonekana kuzozonia hatamu za uongozi.
Bi Mirobi alisema hatua hiyo ina athari za kusababisha mgawanyiko miongoni mwa viongozi hao.
Akizungumza na wanahabari mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Bi Mirobi aliikosoa kamati ya Nairobi iliyochaguliwa kuendeleza kampeni za Jubilee katika ukanda wa Pwani.
Alidai kuwa kamati hiyo imekuwa na ubaguzi na imekuwa ikiwatenga wanachama wa Mombasa.
Wakati huo huo, mwanaharakati huyo ameilaumu kamati hiyo kwa madai ya kuzembea katika utendakazi wake, huku akisema imechangia kushuhudiwa kwa migawanyiko miongoni mwa wanachama.
Kauli ya Bi Mirobi inajiri baada ya kushuhudiwa vurugu siku ya Jumatano wakati wa uteuzi wa viongozi 19 watakaoendeleza kampeni za chama katika maeneo mbalimbali ukanda wa Pwani.