Serikali ya Kaunti ya Mombasa imesema kuwa itawachukulia hatua za kisheria mwanakandarasi na mhandisi wa jengo la kibiashara la Nyali lililoko mjini Mombasa.
Haya yanajiri baada ya sehemu ya choo ya jengo hilo kuporomoka usiku wa kuamkia siku ya Jumatatu.
Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la tukio hilo siku ya Jumatatu, mkuu wa Idara ya Mipangilio Francis Thoya, alimlaumu mwanakandarasi huyo kwa kuruhusu ujenzi wa jengo hilo bila kuangazia hatari yake kwa wakaazi.
“Kama serikali ya kaunti, jukumu letu ni kulinda na kutathmini maisha ya wananchi wetu. Hatuwezi kubali mtu afanye kazi inayohatarisha usalama wa watu wengine. Lazima waliosimamia ujenzi wa jengo hili wawajibishwe,” alisema Thoya.
Aidha, Thoya aliaagiza vyumba vyote vilivyoko upande wa kusini wa jengo hilo vifungwe, hadi usimamizi wa jengo hilo utakapo wasilisha ripoti kuhusiana na ujenzi wake.
Thoya vile vile aliwahimiza wafanyibiashara walio na vyumba vya kibiashara katika jengo hilo kutoingia humo ndani ili kuzuia maafa kutokea.
Hakuna yeyote aliyeripotiwa kujeruhiwa katika mkasa huo.