Angel Mutuku alipofikishwa mahakamani siku ya Jumatatu. Picha/radiorahma.co.ke

Share news tips with us here at Hivisasa

Mwanamke aliyekubali kumkata mumewe sehemu nyeti sasa amekanusha mashtaka hayo katika Mahakama ya Mombasa.

Angel Mutuku anakabiliwa na shtaka la kukata sehemu za siri za mumewe, Stephen Ochieng, mnamo Februari 16 katika eneo la Magongo huko Changamwe.

Mutuku amekanusha mashtaka hayo mbele ya Hakimu Julius Nang’ea, ingawa alikuwa amekubali shtaka hilo hapo awali.

Mwendesha mashtaka Lydia Kagori aliiambia mahakama kuwa Ochieng amewasilisha ombi la kumsamehe mkewe.

“Mlalamishi amewasilisha ombi la kutaka kumsamehe mkewe katika afisi yetu,” alisema Kagori.

Haya yanajiri baada ya Mutuku kutaka kusomewa tena mashtaka yanayomkabili.

Mahakama ilikuwa inatarajiwa kumuhukumu siku ya Alhamisi.

Kesi hiyo itatajwa tena Machi 1.