Mwanamke mmoja amefikishwa katika Mahakama ya Mombasa kufunguliwa mashtaka ya ugaidi.
Feruz Abubakar Hamid, alitiwa mbaroni mnamo Januari 7 katika eneo la Bondeni kwa madai ya kupatikana na vilipuzi vinne, vitambulisho bandia zaidi ya sita, pamoja na vifaa vingine vya kieletroniki.
Hata hivyo, Hamid alikanusha mashtaka hayo mbele ya Hakimu Henry Nyakweba.
Mwendesha mashtaka Eugine Wangila, alidai kuwa mshukiwa huyo alikuwa na lengo la kutekeleza mashambilizi ya kigaidi jijini Mombasa, hasa katika maeneo yenye watu wengi kama vile makanisa na afisi za serikali.
Wangila aliwasilisha ombi mahakamani la kutaka mshukiwa huyo kunyimwa dhamana.
“Huenda mshukiwa akatishia mashahidi wa kesi hii iwapo ataachiliwa kwa dhamana. Naomba abaki chini ya ulinzi mkali wa polisi,” alisema Wangila.
Mahakama itatoa uamuzi wa dhamana leo (Jumatatu).