Mwanamke mmoja anazuiliwa katika kituo cha Polisi cha Likoni baada ya kujaribu kujitoa uhai kwa kujirusha katika kivuko cha feri cha Likoni.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akidhibitisha kisa hicho, afisa mkuu wa polisi eneo la Likoni, Willy Simba, alisema kwamba mwanamke huyo kwa jina la Khadija Abdullah, aliye na umri wa miaka 28, alikuwa akitoka Kisiwani Mombasa kuelekea upande wa Likoni.

Simba alisema kuwa Bi Abdullah aliokolewa na wapiga mbizi waliokua katika eneo hilo baada ya kujitupa katika Bahari Hindi.

Hata hivyo, inaripotiwa kuwa mwanamke huyo alikua akipiga kelele huku akiwasihi wapiga mbizi hao kutomwokoa kwa kuwa alikuwa amechoshwa na maisha.

“Baada ya kuhojiwa kwa muda, Khadija alifichua kwamba alikumbwa na matatizo ya kimapenzi na mumewe alikuwa akimtesa,” alisema Simba.

Khadija atazuiliwa katika kituo hicho hadi siku ya Jumanne atakapofikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kujaribu kujitoa uhai.