Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mahakama moja ya Nakuru imemtoza mwanamke mmoja faini ya shilingi elfu thelathini pesa taslimu baada ya kumpata na hatia ya kuuza pombe haramu.

Hii ni baada ya mshtakiwa huyo, Peris Wanjiru mwenye umri wa makamo, kukiri kuwa alipatikana akiuza lita ishirini za pombe haramu aina ya mnamo tarehe nne mwezi Mei mwaka huu katika eneo la Mwariki viungani mwa mji wa Nakuru.

Licha ya kujitetea kuwa hatarudia tena kosa hilo, hakimu mkuu Nyakundi Maroro wa mahakama ya Nakuru alimtoza faini hiyo ya shilingi elfu thelathini pesa taslimu au kifungo cha miezi sita gerezani.

Tukisalia mahakamani, mwanamume mmoja kwa jina Moses Waweru, mzee wa umri wa makamu alitozwa faini ya shilingi elfu tano au kifungo cha mwezi mmoja gerezani baada ya kupatikana akinywa pombe haramu mnamo tarehe tatu mwezi Mei katika eneo la Mwisho wa Lami viungani mwa mji wa Nakuru.

Hii ni baada yake kukiri shtaka hilo mbele ya hakimu mkuu Nyakundi Jumatano ya tarehe nne mwezi Mei.