Mwanamke mmoja mwenye umri wa makamo anapigania maisha yake katika hospitali moja mjini Naivasha baada ya kudungwa kisu mara kadhaa na mumewe kufuatia mzozo kuhusiana na pesa.

Share news tips with us here at Hivisasa

Walioshuhudia walisema kuwa mume wa mhasiriwa huyo ambaye huuza samaki katika eneo la Kamere kando mwa ziwa la Naivasha alifika hapo akiwa mlevi na kudai pesa.

Na wakati mkewe alimnyima, alichomoa kisu na kumdunga shingoni tukio ambalo lilimwacha hali mahututi.

Kisa hicho kilifanyika Jumatano asubuhi.

Wakaazi pamoja na wafanyibiashara waliokuwa eneo hilo walimpa mwanamme huyo kichapo cha mbwa huku wakitishia kumtekeza kabla ya polisi kufika na kumtia nguvuni.

Mkuu wa tarafa ya Kongoni John Opondo alidhibitisha tukio hilo na kusema kuwa walikuwa wakifanya mipango ya kumsafirisha mwanamke huyo hadi hospitali nyingine ili aweze kufanyiwa upasuaji wa kuondoa kisu hicho shingoni.

Mkuu huyo aidha ameongeza kuwa mshukiwa huyo  ambaye pia yumo hospitalini kufuatia kuchapwa huko atafikishwa mahakamani pindi tu atakapopata nafuu.

"Tuliweza kumuokoa kutoka mikononi mwa umma waliotaka kumteketeza na tumempeleka hospitali tukimzuilia na akipona tutamfungulia mashtaka." Alisema Bw Opondo.