Mwanamke mwenye umri wa makamu anayeshukiwa kumpatiliza kichapo kikali mumewe na hata kumdunga kisu kwenye mgongo mjini Nakuru, alifikishwa mbele ya mahakama ya Nakuru kujibu mashtaka mnamo Jumatatu.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akiwa na mwanawe mchanga mbele ya hakimu mkuu mwandamizi Liz Gicheha, mshukiwa Lucy Wangechi alishtakiwa kwamba mnamo Machi 16, 2016 alimpiga mumewe Isaac Nderitu na kumsababishia majeraha, katika mtaa wa Kwa-Amos kaunti ndogo ya Nakuru Kaskazini.

Mshukiwa Wangechi hata hivyo aliishangaza mahakama baada ya kukiri shtaka, lakini dakika chache baadaye akakana akidai “maelezo sio ya kweli”.

Mahakama ilielezewa kwamba siku hiyo Wangechi alikerwa sana na madai ya jiraniye kwamba alikuwa amehudhuria sherehe ya kula mbuzi iliyofaa kuhudhuriwa na wazee peke yao katika hoteli moja mjini.

Mumewe alikuwa kati ya waliokuwa wamehudhuria sherehe hiyo ila hakumtetea kamwe mkewe wakati alipokemewa na majirani, jambo lililomgadhabisha mshukiwa na kumpatiliza mumewe kichapo.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Mei 23, 2016 itakaposikilizwa tena.