Mwanamume mmoja amefikishwa katika mahakama wa Winam jijini Kisumu kujibu shtaka la kumvamia na kumpiga jirani yake.
Upande wa mashtaka ulielezea mahakama siku ya Jumanne kuwa mshtakiwa, Kennedy Awiti, alimvamia mlalamishi Peter Odongo na kumsababishia majeraha mwilini.
Odongo, ambaye ni mkaazi wa Kasule, jijini Kisumu alieleza mahakama kuwa mnamo tarehe Juni 13, 2014, Awiti alimzaba kofi hali iliyopelekea jicho lake la kulia kupoteza uwezo wa kuona kwa muda wa siku kadhaa huku sikio pia likiziba kwa muda.
Mlalamishi huyo alisema kuwa vurugu hiyo ilizuka baada ya watoto wa Awiti kwenda haja kwenye boma lake, jambo lililomghadhabisha sana na kumtaka mke wa Awiti kuondoa uchafu huo.
Inadaiwa kuwa Awiti aliposikia kuwa Odongo alimwagiza mkewe kusafisha boma hilo, alikasirika na kumvamia mlalamishi huyo.
Mwendesha mashtaka Edward Korir alipendekeza kesi hiyo kutatuliwa nje ya mahakama kwa kuwa wanaohusika ni majirani ambao wamejuana kwa kipindi cha muda mrefu.
Hakimu Benard Kasuvuli aliagiza kesi huyo kutajwa tena tarehe Aprili 19, 2016.