Mwanamume mmoja jijini Mombasa amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kumbaka mtoto mwenye akili taahira.

Share news tips with us here at Hivisasa

Juma Ali Juma, ambaye ni mjomba wa mtoto huyo, alitekeleza kosa hilo mnamo mwezi Februari mwaka huu, katika eneo la Mtongwe huko Likoni.

Juma alikabiliwa na shtaka la pili la kushiriki mapenzi na mpwa wake, ambayo ni kinyume cha sheria kulingana na sheria za dini.

Siku ya Jumanne, Hakimu mkuu katika Mahakama ya Mombasa Tereseia Matheka, alikitaja kitendo hicho kama cha kinyama.

“Kitendo hicho ni cha kinyama na kinakiuka katiba na dini,” alisema Matheka.

Hakimu huyo alivikashifu visa hivyo vya ubakaji vinavyoendela kuongezeka nchini hasa katika ukanda wa Pwani, na kusema jamii inafaa kuwa mstari wa mbele kupinga visa hivyo.

Matheka alisisitiza kuwa hukumu hiyo itakuwa funzo kwa wabakaji nchini.

Mfungwa huyo alipewa siku 14 kukata rufaa.

Kwingineko, mwanamume mwenye umri wa makamu alifikishwa kizimbani kwa kosa la ubakaji wa mtoto wa miaka saba.

Hamisi Mohammed, anadaiwa kutekeleza kitendo hicho mnamo Julai 12, 2016 katika eneo la Mtongwe, Likoni.

Hamisi alikanusha mashtaka hayo mbele ya Hakimu Teresia Matheka.

Mshukiwa huyo aliachiliwa kwa dhamana ya shilingi laki moja na nusu.

Kesi hiyo itasikizwa Agosti 30, 2016.