Watu wanaosambaza pesa bandia kwenye Kaunti ya Nyamira wameonya dhidi ya kuhusiana na kuendesha biashara hiyo haramu.
Hii ni baada ya maafisa wa polisi wa utawala katika Kituo cha polisi cha Kebirigo kumtia mbaroni mwanamume wa umri wa miaka 24 kwenye mkahawa mmoja akiwa na Sh100,000 bandia siku ya Jumatano.
Akithibitisha kisa hicho, kamanda wa polisi wa utawala Bw Douglas Ogechi alisema kwamba jamaa huyo ajulikanaye kama Opande alitiwa mbaroni baada ya mhudumu wa mkahawa huo kuwaarifu polisi kuhusiana na kisa hicho.
"Mshukiwa alitiwa mbaroni na maafisa wa utawala wa kituo cha polisi cha Kebirigo baada ya mhudumu wa mkahawa huo kupokezwa Sh1,000 bandia. Aliwaarifu polisi waliofika kwenye eneo hilo kwa haraka na kumtia mbaroni mshukiwa huyo aliyejaribu kutoweka,” alisema Ogechi.
Mkuu huyo wa maafisa wa utawala aidha aliwashukru wananchi kwa kushirikiana na polisi kuhakikisha kwamba mshukiwa huyo ametiwa mbaroni huku akiwasihi mawakala wa M-Pesa kuwa macho hasaa nyakati za usiku wasije wakalaghaiwa kwa njia kama hiyo.
"Ningependa kuwasihi mawakala wa M-Pesa kuwa macho hasaa nyakati za usiku ili wasije wakalaghaiwa kwa njia kama hii ambayo maafisa wetu wanakabiliana nayo,” alisema Ogechi.
Kwa sasa mshukiwa huyo yuko kwenye kituo cha polisi cha Nyamira akingoja kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kupatikana na pesa bandia na pia jaribio la ulaghai.