Simanzi imetanda katika eneo la Moto viungani mwa mji wa Molo baada ya mwanamume mwenye umri wa miaka 24 kumuua mzee mwenye umri wa miaka 52 baada ya mzozo.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Duru za kuaminika zimeeleza kwamba mshukiwa huyo ambaye ameadhirika pakubwa na uraibu wa bangi alimlazimisha mzee huyo kuvuta msokoto mmoja wa bangi baada ya kukutana naye barabarani alipokuwa akitoka dukani usiku wa kuamkia Jumatatu.

“Huyu muaji alimlazimisha mzee kuvuta bangi na mzee alipokataa alimgonga kwa nyundo mara tatu kichwani na muda mfupi baadaye mzee aliaga dunia,” alisema mmoja wa walioshuhudia.

Mmoja wa waliofika kwenye eneo la tukio na kumkaribia mshukiwa huyo naye pia alivamiwa na kupigwa kwa nyundo hiyo ya mauti kabla ya kunusuriwa na kupelekwa kwenye hospitali ya wilaya Molo akiwa na majeraha mabaya kichwani.

Umati mkubwa wa watu uliojawa na ghadhabu ulifanikiwa kumkamata mshukiwa huyo na kumpatiliza kichapo cha mbwa huku maafisa wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Molo wakimpata akiwa hali mahututi baada ya kupigwa kitutu na umma.

Wakazi hao waliwataka maafisa wa usalama kumwacha mshukiwa kwenye mikono yao huku wakiteta kwamba huenda Jamaa huyo akaachiliwa huru na kuendeleza unyama huo kabla ya kufikishwa kwenye mizani ya sheria.

Mshukiwa huyo alipelekwa kwenye hospitali ya wilaya Molo ambako alihamishiwa hadi hospitali ya mkoa mjini Nakuru kwa matibabu zaidi.