Mwanamume anayedaiwa kumbaka msichana mmoja wa chuo kikuu cha Egerton tawi la Nakuru alifikishwa kwenye mahakama ya Nakuru siku ya Jumatano na kukana shtaka hilo.
Hii ni baada ya mwanamume huyo, Jared Ogembo, kuponea kichapo kutoka kwa wanafunzi wa chuo hicho siku ya Jumanne baada ya kuokolewa na maafisa wa polisi na kupelekwa katika kituo cha polisi cha Bondeni viungani mwa mji wa Nakuru.
Upande wa mashtaka ulidai Ogembo alitekeleza kosa hilo la kumnajisi mischana huyo wa miaka 18 katika bweni la mwanafunzi mmoja lililoko eneo la Shabaab viungani mwa mji wa Nakuru tarehe Septemba 28, 2015.
Ogembo pia anakabiliwa na shtaka la pili la kumkosea msichana huyo heshima kwa kumgusa sehemu zake za siri.
Ogembo alikana shtaka hilo na kujitetea kwa kusema simu iliyo na arafa kati yake na mlalamishi ambayo angetumia kujitetea kwenye kesi hiyo iliibiwa na umati wa wanafunzi uliokuwa na lengo la kumwadhibu.
Hakimu mkuu Liz Gicheha alimwachilia kwa bondi ya Sh100,000 na mthamini wa kiasi sawia.
Kesi hiyo itasikizwa tarehe Novemba 9, 2015.