Mwanamume mmoja amefikishwa katika Mahakama ya Mombasa kujibu shtaka la kujaribu kujitoa uhai.
Mshtakiwa huyo, Patrick Kamau, anadaiwa kujaribu kujitoa uhai siku ya Jumatatu kwa kujirusha baharini kutoka kwa feri aliyokuwa ameabiri kivukoni Likoni.
Hata hivyo, Kamau alikana shtaka hilo mbele ya Hakimu Teresia Matheka siku ya Jumanne.
Mshtakiwa huyo aliambia mahakama kuwa kulikuwa na msongamano katika feri hiyo ya MV Nyayo na alisukumwa na jamaa aliyekuwa ameketi karibu naye.
Aidha, Kamau alieelezea mahakama kuwa bibi na mtoto wake wanamtegemea na hivyo hawezi jaribu kujitoa uhai.
Kiongozi wa mashtaka aliwasilisha ombi la kutaka mshukiwa huyo kuendelea kuzuiliwa hadi siku ya Alhamisi, atakapowasilisha mashahidi wanne mahakamani.