Mwanamume mmoja ameshtakiwa kwa madai ya kuzua vurugu kwenye Kituo cha polisi cha Central, jijini Mombasa.
David Nguti anadaiwa kutaka kumpiga afisa wa polisi katika kituo hicho siku ya Alhamisi, pamoja na kuharibu mali ya ofisi hiyo.
Hata hivyo, Nguti alikanusha mashtaka hayo mbele ya Hakimu Douglas Ogoti.
Hakimu Ogoti aliagiza Nguti kutozwa dhamana ya shilingi elfu 50.
Kesi hiyo itasikizwa tarehe Novemba 7, mwaka huu.
Haya yanajiri miezi michache baada ya wasichana watatu, wanaodaiwa kuwa wanachama wa kundi la al-Shabaab, kuuawa kwa kupigwa risasi baada ya kudaiwa kujaribu kutekeleza shambulizi la kigaidi katika kituo hicho.