Mwanamume mmoja amefikishwa katika Mahakama ya Mombasa kujibu shtaka la kumpiga na kumjeruhi bibi yake.
Upande wa mashtaka ulielezea mahakama siku ya Jumatatu kuwa mshtakiwa, Hassan Rashid, alimpiga bibi yake mnamo tarehe 6 mwezi Aprili, katika eneo la Changamwe, Kaunti ya Mombasa na kumsababishia majeraha.
Mshtakiwa huyo aliambia mahakama kuwa alikuwa na hasira baada ya kugundua kuwa pesa zake shilingi elfu mbili zilikuwa zimepotea, na kushuku kuwa bibi yake ndiye aliyekuwa amezichukua.
Bwana Rashid aliomba mahakama kumsamehe kwa kusema kuwa ana watoto watatu wanaomtegemea.
Hakimu Teresia Matheka aliagiza mshtakiwa huyo kuregeshwa mahakamani tarehe 25 mwezi Mei ili kusomewa hukumu yake.