Huenda shule nyingi za umma katika eneo la bunge la Borabu zikanufaika pakubwa kutokana na mpango wa mwanasiasa wa eneo hilo Nyandoro Kambi kutaka kujenga vyoo katika shule zilizo na uhaba wa vyoo ili kihimili idadi kubwa za wanafunzi.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akihutubu katika shule ya msingi ya Riamanoti siku ya Jumanne, Kambi alisema kuwa mradi huo wa kujenga vyoo vya kisasa almaarufu 'Safisha shule' utasaidia shule nyingi katika eneo hilo kuepukana na magonjwa yanayo sababishwa na uchafu.

"Mradi huu wa kujenga vyoo na hata kupeana bidhaa maalum za kuhifadhi taka katika shule za umma na unaofadhiliwa na wakfu wangu wa Nyandoro Kambi utasaidia pakubwa kuimarisha hali ya uzingatifu wa usafi, hali itakayo waepusha wanafunzi na magonjwa yanayosababishwa na uchafu," alisema Kambi. 

Nyandoro aidha aliongezea kusema kuwa mradi huo utazisaidia shule mbalimbali na zilizo na mahitaji ya juu kwenye wadi zote za eneo bunge hilo, huku akiwahimiza walimu kuzingatia usafi kuhakikisha kuwa wanafunzi wakoikatika hali safi.

"Kuna shule zaidi ya hamsini ambazo tumechunguza na kubaini kuwa zina mahitaji ya kujengewa vyoo kote Borabu na tutahakikisha kuwa shughuli ya ujenzi wa vyoo hivyo inamalizika ifikapo mwezi mei mwaka huu," aliongeza Kambi.