Mwanasiasa Ogeto Swanya kutoka eneo bunge la Kitutu Masaba ameapa kuendelea kuwasaidia mayatima wa eneo bunge hilo kupata elimu.
Akiongea Ijumaa katika hafla ya mazishi ya mama Mary Simeon kijiji cha Riamisiani wadi ya Gesima Ogeto alisema anataka kuinua kiwango cha masomo katika eneo bunge hilo.
“Tunataka kila mmoja wetu aweze kuendeleza maisha yake bila matatizo. Kuwasaidia watoto wapate elimu ni njia moja ya kufanya maisha yao yawe bora,” akasema Ogeto.
Aidha, aliwaomba wakazi wote kushirikiana ili kuinua viwango vya masomo kwa kuwa ndio itasaidia kupata viongozi wa kesho.
Ogeto alisema kuwa atatembelea shule zote katika eneo hilo huku akiwatabua watoto mayatima.
Kwa upande mwingine aliwaomba viongozi waliomamlakani kwa sasa kuwasaidia wananchi ili kuinua viwango vya maendeleoo katika eneo bunge la Kitutu Masaba.
Alimwomba mwakilishi wa wadi ya Gesima Kennedy Nyameino kukarabati baadhi ya barabara ambazo zimeharibika katika wadi ya Gesima ili kuwasaidia wakulima na wafanyibiashara.
Ogeto pia alidokeza kuwa ameongea na Nyameino kuhusu ukarabati wa barabara ya Matunwa –Kiamitengi na ile ya Gesima – Esani- Magombo.