Baada ya majaji wa mahakama ya kimaita inayoshughulika kesi za jinai ICC kutupilia mbali kesi iliyokuwa ikimkabili naibu rais William Ruto na mtangazaji Joshua Sang, mwaniaji wa cheo cha ubunge katika eneo bunge la Mugirango kaskazini Jason Mosinga amejitokeza kuwarahi wakenya kuheshimu maamuzi ya mahakama hiyo. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Akihutubu kwenye hafla moja ya mazishi kule Nyamusi katika wadi ya Bokeira siku ya Alhamisi, Mosinga alisema kuwa yafaa wakenya waheshimu uamuzi wa majaji wa mahakama hiyo na kuwahimiza kukumbatia amani. 

"Kwa maana majaji wa mahakama ya ICC tayari wameamua kwamba hamna ushahidi wa kutosha kuruhusu kesi za Ruto na Sang kuendelea sasa yafaa wakenya waheshimu uamuzi huo na kukumbatia amani na utangamano," alisema Mosinga. 

Mosinga aidha ameitaka serikali ya kitaifa kuchukua hatua za kuhakikisha kwamba waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka wa 2007 wanafidiwa.

"Kwa miaka nane iliyopita tangu kuzuke ghasia za uchaguzi nchini, bado kungali na wakenya wanaoishi kwenye mahema ambao wangali kufidiwa na tunajua wazi kwamba serikali ilitenga kiasa fulani cha pesa ili kuwafidia waathiriwa ila wengi wao hasa hapa gusii bado wangali kufidiwa na ili haki itendeke sharti wafidiwe ndio taifa hili lisonge mbele," aliongezea Mosinga.