Mgombea wa kiti cha uwakilishi wa wanawake Kaunti ya Mombasa Bi Zamzam Mohammed ameilamu Tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC, kwa kile alichokitaja kama kushindwa kuwajibikia majukumu yake kikamilifu.
Akizungumza na wanahabari mjini Mombasa, Bi Zamzam alisema kwamba idadi kubwa ya mashine za kusajili wapiga kura zimeonekana kukumbwa na hitilafu na kupelekea wakaazi wengi kurudi nyumbani bila kusajiliwa.
Zamzam aidha amesema ni jambo la kushangaza kupata mashine hizo kwenye vituo mbalimbali hazifanyi kazi, na kutaka swala hilo kushughulikiwa haraka.
Mwanasiasa huyo vile vile amedokeza kwamba itakuwa ni vyema zaidi iwapo tume hiyo itaongeza muda zaidi wa zoezi hilo, ili kuwapa wananchi nafasi ya kujiandikisha.
Aidha, ameitaka tume hiyo kuwahamasisha wananchi kuhusu zoezi hilo.
Zamzam alisema kuwa idadi kubwa ya wananchi hawafahamu vyema umuhimu na jinsi gani ya kusajiliwa kama wapiga kura.
Hata hivyo, amewahimiza wakaazi wa Mombasa kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo kwa kuwa ni haki yao kikatiba kusajiliwa kama wapiga kura.