Gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama amepewa changamoto kuzungumzia swala la barabara za eneo bunge la Mugirango magharibi kuwa katika hali mbaya.
Akizungumza kwenye kijiji cha Kiambere katika wadi ya Bosamaro, mwanasiasa Peter Oire alisema kuwa serikali ya kaunti ya Nyamira ingali kujibu barua aliyoiandikia kulalamikia hali mbaya ya barabara za eno hilo.
"Wakulima huwa na wakati mgumu kusafirisha mazao yao kwenda sokoni kutokana na hali mbaya ya barabara, na gavana Nyagarama bado hajatujibu kuhusiana na hali hii hata baada ya kumwandikia barua ya kulalamikia barabara mbovu," alisema Oire.
Mwanasiasa huyo ametishia kuwaongoza wakulima wa eneo hilo kwenye maandamano hadi kwenye afisi kuu za kaunti kwa wiki moja ijayo iwapo lalama zao haziwezi shughulikiwa.
"Serikali ya kaunti ina wiki moja tu kushughulikia matakwa yetu kwa kuwa tunayodai ni haki yetu na tuna mipango ya kufanya maandamano hadi kwenye afisi kuu za kaunti ya Nyamira," alitishia Oire.
Kulingana na Oire, eneo bunge la Mugirango magharibi halikunufaika pakubwa kutokana na mpango wa serikali ya kaunti kulima kilomita 240 za barabara kwenye kaunti ya Nyamira.
"Nimesafiri kote Nyamira na nimegundua kuwa eneo bunge la Mugirango magharibi halikunufaika pakubwa na mradi wa serikali kukarabati kilomita 240 za barabara kote Nyamira," alisema Oire.