Kufuatia wazazi na walezi kulalamikia vikali bei ya vitabu vya kusoma shule zinapofunguliwa, mwanasiasa wa Borabu Nyandoro Kambi amesema kwamba serikali inastahili kutafuta mwafaka wa kuwatoza kodi zisizo za juu wachapishaji vitabu. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Akihutubu katika eneo la Borabu siku ya Jumapili, Kambi alishtumu muungano wa wachapishaji vitabu na serikali ya kitaifa kwa kuto fikia mwafaka wa kutozwa kodi muungano huo, hali aliyosema imewafanya wazazi na walezi kushindwa kuwanunulia wanafunzi vitabu vya kusoma. 

"Sekta ya uchapishaji wa vitabu vya kusoma ni muhimu sana kwa ukuaji wa elimu nchini, lakini ni jambo la kushangaza kubaini kuwa wachapishaji vitabu wanaendelea kuuza vitabu hivyo kwa bei za juu kutokana na kuwepo kwa tofauti kali baina yao na muungano wa wachapishaji vitabu kuhusiana na viwango vya kodi," alisihi Nyandoro. 

Kambi aliongeza kusema kuwa shule nyingi za umma zilifanya vibaya kwenye matokeo ya mtihani wa darasa la nane KCPE kutokana na kutokuwepo kwa vitabu vya kusoma vya kutosha katika shule husika akisisitiza kuwa sharti serikali ichukue hatua kupunguza kiwango cha kodi hiyo.

"Hizi bei mpya za ununuzi wa vitabu vya kusoma zinawaathiri sana wanunuzi kwa kuwa hatuwezi nunua vitabu vya kusoma kwa watoto wetu kwa maana kuna shule huku Borabu ambazo hazijafanya vizuri na huenda ikawa ni kwa sababu ya ukosefu wa vitabu vya kusoma," aliongeza Nyandoro.