Mwanasiasa kutoka eneo bunge la Borabu ameitaka kamati iliyochaguliwa katika Kaunti ya Nyamira kuchunguza matokeo ya mtihani wa KCPE yaliyotupiliwa mbali kufanya uchunguzi huo haraka.
Haya yanajiri baada ya matokeo ya shule tatu za msingi kutupiliwa mbali baada ya matokeo hayo kutangazwa hivi maajuzi na Waziri wa Elimu nchini Fred Matiang’i.
Akizungumza siku ya Jumatano katika eneo bunge la Borabu, Nyandoro Kambi aliomba uchunguzi huo kufanywa haraka iwezekanavyo ili wakaazi wa Kaunti ya Nyamira kujua kilichopelekea matokeo hayo kutupiliwa mbali.
“Naomba kamati iliyochaguliwa kufanya uchunguzi wa matokeo yaliyotupiliwa mbali kufanya haraka ili tujue ni nini haswa kilichopelekea matokeo ya shule tatu kutupiliwa mbali,” alisema Kambi.
Shule zilizoathirika katika Kaunti ya Nyamira ni Akademia ya Nyangena, Shule ya msingi ya Matutu na Shule ya msingi ya Mokomoni.
Wakati huo huo, Kambi aliomba walimu kutia motisha wanapowafunza watoto na kutojihusisha na visa vya wizi wa mitihani.
“Naomba walimu muwe mnawafunza wanafunzi kwa bidii ili kuwawezesha kupita katika mitihani ya kitaifa na kuepuka na visa vya wizi,” alisema Kambi.