Mwanasiasa na mfanyabiashara maarufu wa eneo la Kisauni Ali Mbogo, ameshtumu tukio ambalo alivamiwa na kundi la Wakali Kwanza mjini Mombasa.

Share news tips with us here at Hivisasa

Mbogo aliyekuwa akiwahutubia wakaazi katika eneo la Kisauni baada ya kuwakabidhi wanafunzi hundi za ufadhili wa masomo, alisema kwamba inasikitisha mno kwa mahasimu wake wa kisiasa kuwatumia vijana kutekeleza uhalifu.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatano, Mbogo alisema kwamba tukio hilo sio la kuridhisha na ni sharti mahasimu wake wa kisiasa kukubali upinzani na kuendeleza siasa zao pasipo na vurumai lolote.

Mwanasiasa huyo amewahimiza wakaazi wa eneo hilo la Kisauni kuwachagua viongozi kulingana na mienendo yao, na kufanya maamuzi ya busara katika uchaguzi mkuu ujao.

Mbogo aidha alisema kwamba eneo hilo la Kisauni limekumbwa na uongozi duni kwa muda sasa.

"Ninawaomba wakaazi wa eneo hili la Kisauni kuwachagua viongozi waadilifu na kukoma kuhusishwa katika visa vya kihalifu ili eneo la Kisauni kuwa salama,” alisema Mbogo.

Mbogo ambaye tayari ameweka bayana azma yake ya kuwania ubunge wa Kisauni katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao, amesema kwamba kamwe hatatishwa na uvamizi huo na ataendelea kupigania maslahi ya wakaazi wa Kisauni.