Mwanasiasa Joshua Onduko wa Nakuru anahofia usalama wake akidai kuna watu wanaotaka kumuangamiza.
Katika mahojiano Jumapili, Onduko alisema kuna watu waliojaribu kuteketeza makazi yake, lakini juhudi zao zikatibuka.
Kwa mujibu wake, huenda hatua hiyo ni kutokana na hatua yake kutangaza azma ya kuwania kiti cha wadi ya Kapkures Nakuru.
"Kuna baadhi ya watu wanaojaribu kuniangamiza kisiasa lakini nimepiga ripoti kwa maafisa wa polisi na natumai hatua mwafaka itachukuliwa," alisema Onduko.
Wakati huo huo alitoa wito kwa wapinzani wake kuepuka siasa potovu za ukabila na za kugawanya wananchi akiongeza kuwa wakati huu ni wa siasa komavu za maendeleo.