Kufuatia waziri mpya wa ardhi Jacob Kaimenyi kuzuru eneo la Pwani mapema wiki hii, kiongozi mmoja wa kisiasa anamtaka waziri huyo kuonyesha vitendo kwa kutekeleza yale aliyowahidi alipokuwa katika eneo hilo siku ya Jumatatu.
Akiongea siku ya Jumatano katika afisi yake jijini Mombasa, Raymond Mkala, ambaye anapania kuwania kiti cha uwakilishi wadi katika eneo la Kongowea katika Kaunti ya Mombasa alisema kuwa waziri Kaimenyi sharti aanze kazi yake ili kuona kuwa matatizo wakazi wa Pwani wanapitia kuhusiana na ardhi yanapata utatuzi wa kudumu.
Aidha alimtaka kuonyesha vitendo, huku akimshukuru kwa kuanzia ziara yake ya kwanza kama waziri katika eneo la Pwani ambalo lina visa vingi vya dhuluma vya mashamba na ardhi kwa jumla.
Alimtaka waziri huyo kuhakikisha kuwa anamshirikisha mwenyekiti wa tume ya ardhi nchini Mohamed Swazuri ili kunufaisha waathiriwa na kuleta mwafaka na suluhisho la kutegemeka hasa masuala na kesi nyingi zinazohusuana na ardhi si tu eneo la Pwani bali kote nchini.
Muwaniaje huyo aliongeza kuwa kuna haja ya kulainisha idara zote chini ya wizara ya ardhi ili kuleta uuwiano miongoni mwa masuala ambayo yamekuwa kikwazo kwenye wizara hiyo kama vile ufisadi na unyakuzi wa mashamba ya watu binafsi na yale ya serikali na mashirika kwa kushirikiana na wanasiasa ambao nia yao ni kufaidi kutoka kwa wengine.