Biwi la simanzi limetanda eneo la Mai Mahiu eneo Naivasha baada ya seremala mmoja mwenye umri wa miaka ishirini kujitoa uhai saa chache baada ya kukosana na mpenziwe.
Mwendazake aliyekuwa amekunywa kemikali yenye sumu alikimbiziwa katika hospitali kuu ya wilaya ya Naivasha baada ya hali yake kuzorota, na kuaga dunia alipokuwa akitibiwa.
Wakazi wa eneo hilo wamesema kuwa mwendazake aliamua kufanya kitendo hicho baada ya kumpata mpenziwe ambaye ni mjakazi akimbusu mwanamume mwingine.
Mkazi mmoja John Ngure amesema kuwa wawili hao wamekuwa wapenzi kwa muda sasa na haijulikani kilichomfanya msichana huyo kutoka nje ya mapenzi hayo.
"Majirani walimkimbiza katika hospitali moja hapa Mai Mahiu na wakati hali yake ilianza kudhoofika wakaamua kumpeleka mjini Naivasha ambako alifariki baadaye." Akaongeza Bw Ngure.
Afisaa mmoja wa polisi ambaye hakutaka kutajwa jina lake amedhibitisha tukio hilo na kusema kuwa mwili wa mwendazake umepelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali kuu ya wilaya hiyo.