Wimbi la simanzi lilitanda katika kitongoji cha Arash katika kaunti ndogo ya Subukia, baada ya mwanamume mwenye akili punguani kufariki, alipojirusha mbele ya gari lililokuwa kwenye mwendo wa kasi kwenye barabara ya Nakuru kwenda Nyahururu Ijumaa jioni.
Walioshuhudia tukio hilo karibu na shule ya upili ya Subukia walisema marehemu, aliye tambulika kama Samuel Mureithi aliye na umri wa miaka 32, anaishi katika kijiji cha Arash na ameishi na matatizo ya kiakili kwa mda.
Akidhibitisha tukio hilo, Kamanda mkuu wa Subukia Alex Ng’ang’a alisema mwendazake alijirusha mbele ya gari hilo aina ya Toyota Prado lililokuwa katika mwendo wa kasi, na akapata majeraha mabaya.
Ng’ang’a alisema kuwa alikimbizwa katika hospitali ya kaunti ndogo ya Nyahururu, lakini akafariki masaa machache baadae.
Kinara huyo wa polisi aliongezea kuwa gari hilo ambalo lilikuwa likiendeshwa na mwenyewe Samuel Ikumbu wa miaka 65 lilizuiliwa katika kituo cha polisi cha Subukia, na kisha likafanyiwa ukaguzi kabla ya kuachiliwa.
“Mwili huo utafanyiwa upasuaji ili kubaini kiini cha kifo,” alisema bwana Ng’ang’a.