Mmoja wa wawaniaji wa ubunge katika eneo bunge la Borabu Daktari Nyandoro Kambi sasa amejitokeza kuitaka tume ya kukabili ufisadi nchini EACC kufunga akaunti za benki za washukiwa waliotajwa kuhusika na uvujaji wa millioni 791 kutoka kwa hazina ya shirika lakitaifa la vijana.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Kulingana na Kambi, yafaa tume ya EACC izifunge akaunti zote za benki za washukiwa hao ili kuipa nafasi tume hiyo kuwachunguza washukiwa bila ya muingililio wa aina yeyote. 

"Hii sakata ya uvujaji wa mamilioni ya pesa kutoka kwa shirika la NYS inaelekea kuwachosha wakenya kwa maana tumekuwa tukisikia tume ya EACC ikiwahoji washukiwa bila ya hatua mwafaka kuchukuliwa dhidi yao, na ndio maaana tunataka tume hiyo kuzifunga akaunti zote za benki za washukiwa waliotajwa hadi pale uchunguzi dhidi yao utakapokamilika," alisema Kambi.

Kambi aidha alisema kuwa kufungwa kwa akaunti za benki za washukiwa hao itasaidia tume ya kukabili ufisadi nchini kuchunguza suala hilo bila kuingililiwa kivyovyote, huku akiipa changamoto tume hiyo kuhakikisha kuwa wanasiasa wote waliotajwa wanahojiwa na hatua kuchukuliwa dhidi yao. 

"Kitu ambacho wakenya wanataka kujua ni watu waliovuja millioni 790 kutoka kwa shirika la NYS na kwa kuwa baadhi ya wanasiasa wametajwa kuhusika, yafaa akaunti zao za benki zifungwe ili wasiingililie uchunguzi wa tume ya EACC," aliongezea Kambi.