Mbunge wa Matuga Hassan Mohamed Mwanyoha amewashutumu wabunge waasi wa chama cha ODM wanaotoka katika mkoa wa Pwani na kuwataja kama viongozi wanaojali maslahi yao ya kibinafsi badala ya wananchi waliowachagua.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza katika eneo bunge lake siku ya Jumatano, mbunge huyo, alisema hatua ya baadhi ya wabunge waliochaguliwa kwa tiketi ya chama cha ODM kutangaza kukihama chama hicho na kujiunga na mrengo wa Jubilee ni ishara tosha kuwa hawana nia ya kuwafanyia kazi wananchi bali kujinufaisha kisiasa.

''Tunawajua vizuri sana, wananjaa ya pesa sasa wameenda Jubilee ili wapewe mgao, lakini wacha niwaambie ODM bado iko imara na haiwezi linganishwa na chama kingine nchini,'' Mwanyoha alisema.

Mwanyoha aliwataka wabunge hao kujiuzulu ili kutoa nafasi kwa uchaguzi kufanywa katika maeneo bunge yao kwani tayari wamekihama chama kilichowapeleka bungeni.

Kauli ya Mwanyoha inajiri wakati idadi ya wabunge wa mkoa wa Pwani wanaotangaza kuuhama mrengo wa Cord na kujiunga na chama kipya cha JAP ikizidi kuongezeka.

Mbunge wa Likoni Masoud Mwihima na Gideon Mung'aro wa Kilifi Kaskazini ni miongoni mwa wabunge waliotangaza kukihama ODM na kujiunga na Jubilee.