Mbunge wa Lunga Lunga Khatib Mwashetani katika hafla ya awali. [Picha/ standardmedia.co.ke]
Wakaazi wa Kwale wamehimizwa kujitokeza kwa wingi kumchagua Raisi Uhuru Kenyatta katika marudio ya uchaguzi wa urais.Mbunge wa Lunga Lunga Khatib Mwashetani amewahimiza wakaazi kumchagua Rais Kenyatta kwa muhula wa pili kwa kusema kuwa serikali ya Jubilee imeleta maendeleo katika kaunti hiyo.“Jubilee imetuletea miradi mingi ya maendeleo kinyume na mrengo wa NASA unavyodai. Nawaomba mujitokeze kwa wingi tumchague Uhuru tena,” alisema Mwashetani.Akihutubia makundi ya wanawake katika eneo la Kikoneni, Mwashetani alisema serikali ya Jubilee inajali maslahi ya wananchi hasa wanawake.“Kuna miradi mingi ya wanawake iliyoanzishwa na Jubilee Kwale na kote nchini kwa jumla, kinyume na serikali zilizopita. Jubilee imejitahidi na inastahili kupongezwa,” alisema Mwashetani.Aidha, Mwashetani alisema kuwa iwapo kinara wa upinzani Raila Odinga atashinda katika uchaguzi huo, Gavana wa Kwale Salim Mvurya atakuwa na wakati mgumu kufanikisha malengo yake.“Chageuni Uhuru ili gavana wetu apate nguvu ya kutekeleza majukumu yake kwa wakaazi wote wa Kwale,” alisema Mwashetani.Mwashetani aidha alipuzilia mbali maandamano ya NASA na kuyataja kama yasiyokuwa na umuhimu wowote kwa Wakenya.Amewataka vijana kutokubali kutumiwa na NASA kufanikisha maandamano hayo.“Watoto wao wako nchi za nje lakini wanatumia watoto wetu katika maandamano yasiyokuwa na msingi,” alisema Mwashetani.