Wawekezaji wa sekta ya utalii katika Kaunti ya Mombasa huenda wakapoteza wateja wao na utalii kuathirika iwapo zogo linaloendelea kushuhudiwa katika kivuko cha Likoni halitapata suluhu ya mapema.
Kulingana na raia mmoja kutoka Italia ambaye amekuwa mwekezaji mkubwa katika sekta hiyo na ambaye amekuwa mtalii katika nchi ya Kenya kwa miaka zaidi ya 20, sharti serikali ya nchi yoyote kuwajibikia vitengo ambavyo huwaletea mapato, badala ya kuendelea kufanya unyonge jinsi inavyoshuhudiwa kwa sasa.
Katika mahojiano siku ya Jumanne mjini Mombasa, Johan Demaros, ambaye amekuwa akiwaleta baadhi ya raia kutoka nchi yake ya Italia na kuja humu nchini nyakati za baridi, hana nia tena ya kualika wageni hadi hali ibadilike au aanze kubadili na kuelekea nchi jirani ya Tanzania.
Demaros, ambaye pia amewekeza katika sekta ya uchukuzi; hususan kwenye gari za kukodi za kuwabeba watalii kutoka jiji Mombasa alisema kuwa amepata hasara kubwa tangu eneo la kivuko cha Likoni kuanza kushuhudia pandashuka za feri kukwama.
“Kama juzi pekee niliweza kupoteza zaidi ya wageni mia mbili ambao walikuwa wanataka kuzuru katika fuo za Pwani ya kusini huko Diani kwa sababu hakukuwa na feri za kutosha kuvusha magari pamoja na wenyeji, hata wale tayari nilikuwa nimepanga walikaa kwenye kivuko hicho kwa zaidi ya saa tatu,” alisema Demaros.
Kwenye mtatariko huo, wengi wa watalii ambao walitarajiwa kuwasili kwenye uwanja wa ndege walikosa nafasi hiyo kwa kukaa kwenye msongamano na kuchelewa.