Hatima ya Muungano wa Jumuiya ya kaunti za Pwani haijajulikana kufikia sasa huku kukiwepo na tetesi kwamba muungano huo huenda ukawa umefifia kwa kile kinachoonekana kama mgawanyiko na kutoelewana miongoni mwa viongozi kutoka eneo la Pwani.
Mwezi jana, baadhi ya viongozi kutoka Pwani walijitokeza na kupinga muungano huo huku wakidai kuwa muungano huo umekufa.
Mnamo Machi 29, mwenyekiti wa Wabunge kutoka eneo la Pwani Gunga Mwinga ambaye alichukuwa nafasi ya Gideon Mung’aro alisema kuwa muungano huo ulianza kwa wingi wa ahadi kwa wakazi wa Pwani lakini kufikia sasa hakuna lolote ambalo limetizwa.
Kwa upande wao, wakazi wa Pwani haswa katika Kaunti ya Mombasa wamekubaliana na Mung’aro kuwa magavana wanastahili kueleza jinsi muungano huo unavyotumia fedha zao, huku wakisema kuwa muungano huo utawasaidia kwani viongozi wao wanawaelewa zaidi kuliko mtu yeyote.
Wakazi hao aidha wamesema kuwa iwapo wenzao wa kaunti nyengine hawatakuwa waangaligu, huenda uhusiano mwema uliopo baina ya kaunti za Pwani ukaharibika kwani huu ni wakati ambao kila mmoja anapiga siasa, hivyo basi kuwataka kuwa makini.
Muungano huo ambao uliwapa matumaini wakazi wa Pwani ya kuona na hata kushuhudia maendeleo mashinani ulionekana kuyumbayumba Mung’aro alipodai kuwa ulikuwa wamanufaa kwa viongozi kadhaa.
Kauli hiyo ilipingwa vikali na Gavana wa Mombasa Hassan joho na mwenzake wa Kwale Salim Mvurya waliosema kwamba muungano huo upo imara na kuwa viongozi wa kaunti sita ikiwemo ya Mombasa, kilifi, Kwale, Taita Taveta, Lamu na Tana River wamekuwa wakijadiliana kuhusu jinsi watakavyoafikia ajenda zao.