Bunge la kaunti ya Mombasa siku ya Jumatano liliidhinisha hoja inayotoa makataa ya miezi 3 kwa kampuni inayochoma lami katika wadi ya Airport kufungwa.
Hii ni baada ya kamati maalum ya afya na mazingira kupewa jukumu la kutembelea wakaaazi wa eneo hilo na kuandaa ripoti waliyoiwasilisha bungeni kujadiliwa.
Spika wa kaunti hiyo Thadius Rajwai ameidhinisha hoja hiyo inayosema kuwa kampuni hiyo inatakiwa kuhamia eneo la viwanda badala ya makaazi ya watu.
Wakaazi wa eneo hilo wanalalamikia moshi unaotoka katika kiwanda hicho na wanasema kuwa umeathiri afya yao kwani wamekuwa wakikohoa kila mara, huku pia wakisema kelele zinazotoka katika kiwanda hicho wakati wa usiku zinawanyima usingizi
Mwakilishi mteule katika bunge hilo ambaye pia ndiye aliyewasilisha hoja hiyo bungeni Mary Akinyi aliambia mwandishi wetu kuwa amepanga kuandaa mkutano na wakaazi hao ili kuwaeleza yale yaliyojadiliwa bungeni kuhusu swala hilo.
“Mimi nitapigania haki ya wakaazi hao kwa sababu hata mimi naishi katika eneo hilo na hali hiyo pia inaniathiri, nitafanya mkutano nao ili niwaeleze kile tumeongea leo,” alisema Akinyi.